Thursday, July 31, 2014

SIKILIZA RIPOTI YA HALI YA HAKI ZA BINADAMU KWA KIPINDI CHA NUSU MWAKA JANUARI – JUNI 2014



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - HALI YA HAKI ZA BINADAMU KWA KIPINDI CHA NUSU MWAKA
JANUARI – JUNI 2014

Ndugu waandishi wa habari
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kinaendeleza utaratibu wake wa kila mwaka wa kutoa tathmini ya hali ya haki za binadamu kwa kipindi cha miezi sita. Tathmini hii hufanywa kwa malengo ya kutoa muelekeo wa hali ya ulinzi na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Taarifa hizi ni matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, ufuatiliaji wa ukiukwaji wa haki za binadamu, pia taarifa mbali mbali toka kwa waangalizi wa haki za binadamu, wasaidizi wa kisheria, taarifa rasmi toka taasisi za Serikali, Bunge, Mahakama, vyombo vya habari na asasi mbali mbali zisizo za kiserikali.

Katika kipindi cha miezi sita, tathmini ya hali ya haki za binadamu imezingatia hali halisi ya tabia na hali ya watu kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kama ilivyotolewa na mtakwimu mkuu. Takwimu za sensa ya watu na makazi inaonyesha wanawake kuwa wengi kuliko wanaume, idadi ya wanawake ni asilimia 51.3 na wanaume ni asilimia 48.7. Lakini bado idadi ya wanawake katika vyombo mbalimbali vya maamuzi na fursa nyinginezo mbalimbali bado ipo chini ukilinganisha na wanaume. Bado mwanamke ni mhanga mkubwa wa vitendo vya ukatili wa majumbani na ubakaji kama takwimu za nusu mwaka zinavyosema, mpaka kufikia Juni mwaka huu 2014 wanawake na wasichana 2878 walibakwa, vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana vile vilivyoripotiwa polisi nchi nzima vilikuwa 3,633.
Taarifa hii ya sensa ya watu na makazi pia inaonyesha kwamba, idadi kubwa ya watu wanaishi vijijini. Licha ya kuwa na idadi kubwa ya wananchi wanaoishi vijijini bado huduma za jamii kama upatikanaji wa maji, huduma za afya, shule pamoja na umeme vijijini ni duni. Takwimu zinaonesha, bado vijijini kuna makazi duni ya wananchi kutoka na gharama kubwa za saruji na vifaa vya ujenzi. Mfano katika suala la upatikanaji maji makazi 3,959,857 yanatumia vyanzo vya maji visivyo salama ukilinganisha na makazi 1,902,244 yanayotumia maji ya bomba nchi nzima.
Idadi ya wananchi wengi wapatao 11,359,090 wanategemea kilimo kama shughuli kuu ya uchumi. Hata hivyo wakulima wengi bado wanatumia jembe la mkono. Uwekezaji katika mashamba makubwa wamepewa wawekezaji wakubwa, Mfano: Mashamba makubwa ya Mpunga yaliyokuwa ya shirika la NAFCO huko wilayani Mbarali-Mbeya wamepewa wawekezaji na wakulima wazawa wametengewa maeneo yasiyofaa. Hii huchochea migogoro ya mara kwa mara ya ardhi katika wilaya hiyo ya Mbarali.
Kiwango cha Elimu bado kipo chini sana katika nchi. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi idadi ya watanzania waliopata elimu rasmi ni watu 14,495,447. Kati yao watu 11,848,323 wamehitimu elimu ya msingi na wenye elimu ya chuo kikuu ni watu 337,881 tu. Hii ni changamoto kubwa katika kulinda na kuheshimu haki za binadamu. Tafiti zetu mbalimbali zimeonyesha kwamba ongezeko kubwa la watu kujichukulia Sheria mikononi, mauaji yanayotakana na imani za kishirikina, mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ni matokeo ya uelewa mdogo wa wananchi juu ya haki za binadamu. Pia zinachangiwa na kukoseka kwa elimu ya haki za binadamu katika mifumo yetu ya elimu. Kwa mfano kwa kipindi cha nusu mwaka watu 320 wameuawa kwa imani za kishirikina ukilinganisha na watu 303 kwa kipindi kama hiki mwaka 2013. Hii inaonesha kuna ongezeko la matukio haya, idadi ya watu waliouawa na wananchi wanaojiita wenye hasira kali matukio 473 yameripotiwa ukilinganisha na matukio 597 mwaka 2013 ambapo kitakwimu inaonesha kupungua, matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yameanza kuongezeka pia kwa kipindi cha miezi sita iliyopita ambapo watu 2 wameripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa vibaya.
Wananchi kuvamia vituo vya polisi na kusababisha vifo na hasara kubwa ya mali pia matukio haya yameendelea kuripotiwa ambapo kwa kipindi cha miezi sita vituo vitatu vya polisi vilivamiwa na wananchi na kusababisha vifo kwa askari 2 na mgambo 1. Pia jumla ya askari sita waliouawa katika matukio ya uhalifu.
Matukio ya ajali za barabarani yameendelea kutokea kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ubovu wa vyombo vya usafiri, miundo mbinu mibovu, na uzembe wa watumiaji wa barabara. Kwa mwaka huu 2014 katika kipindi cha miezi sita watu 1505 walipoteza uhai (Wanaume 1292 na wanawake 213).
Haki ya kuwa na familia ni moja ya haki za binadamu. Takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha kwamba jumla ya watu 12,570,491 wameoa na kuolewa, 8,730,828 hajaoa wala kuolewa, watu 1,578,568 wanaishi pamoja, watu 232,415 wametengana, watu 715,447 wameachana, wajane 765,284 na yatima ni 1,696,349. Takwimu hizi zinatuelekeza kuna wajibu mkubwa sana wa kulinda na kuheshimu haki hii ya kuwa na familia bora. Katika kipindi cha miezi sita tumeona matukio mengi ya kikatili dhidi ya wanafamilia katika matukio mbalimbali dhidi ya watoto na wanawake. Mfano: Matukio ya kikatili dhidi ya wanawake yanayohusiana na mahusiano ya kimapenzi Mbeya peke yake wanawake 26 waliuawa katika mahusiano haya, pia mauaji yaliyodumu kwa muda huko Butiama suala la mahusiano pia linatajwa kama moja ya sababu ambapo watu 10 waliuawa. Huko Geita wanawake 27 wameripotiwa kuuawa katika matukio ya namna hiyo.
Matukio ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa kwa kiwango kikubwa, ikiwa ni pamoja na kuibuliwa kwa watoto wanaofanyiwa ukatili na kufichwa ndani kama ilivyotokea kwa mtoto wa mmoja mkoani Morogoro ambaye alifariki siku chache baadaye.

Haki ya kuishi katika mazingira safi na salama ni changamoto kubwa ambayo inachochewa na uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na shughuli za binadamu. Mfano bado idadi kubwa ya kaya Tanzania zinatumia nishati ya kuni kwa kupikia. Takwimu za watu na makazi zinaonyesha kwamba, kaya 6,353,229 wanatumia kuni, kaya 2,381,837 wanatumia mkaa, na wale wanaotumia nishati mbadala kama mafuta ya taa ni kaya 225,270, umeme 158,987 tu. Hivyo basi ipo haja ya Serikali kupunguza kodi na kuhimiza matumizi ya nishati mbadala ili kulinda na kuhifadhi misitu yetu
Migogoro ya ardhi, Tafiti ndogo juu ya migogoro ya ardhi nchi inaonyesha kuna changamoto nyingi za ardhi nchini. Utafiti katika wilaya mbali mbali zilizotembelewa kama vile Mvomero, Kilosa, Kilombero, Mbarali, Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Babati na Kiteto inaonyesha bado kuna changamoto kubwa juu ya umiliki, usimamizi na matumizi ya ardhi. Migogoro hii ni baina ya wawekezaji na wananchi, wafugaji na wakulima, wananchi na Serikali pia wilaya na wilaya mfano wilaya ya Longido na Arumeru vijijini vinavyopakana vimekuwa na migogoro ya mipaka ya mara kwa mara. Migogoro hii hupelekea maafa kwa jamii na kwa taifa kwa ujumla, mfano wilayani Kiteto mwanzoni mwa mwaka 2014 yalipotokea mapigano makali na kusababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali.
Usimamizi na utoaji haki, bado kuna changamoto kubwa, mfano idadi ya majaji wa mahakama ya Rufani bado ni ndogo ukilinganisha na idadi ya kesi kwa mwaka. Kwa sasa mahakama ya rufani ina majaji 16 tu, na mahakama kuu ina majaji 69. Idadi hii bado ni ndogo ukilinganisha na idadi ya watumia huduma za mahakama. Katika mahakama za wilaya na mahakama za mwanzo idadi ya mahakimu ni ndogo pia ukilinganisha na idadi ya mahakama zilizopo nchi nzima. Idadi ya mahakimu kwa sasa ni 672 wakati mahakama za mwanzo pekee ni 960.
Hali ya uchakavu wa Mahakama nyingi za mwanzo ni tatizo linalochelewesha utoaji haki na linaongeza gharama za uendeshaji wa mashauri mbalimbali hususani ya jinai. Mfano kati ya mahakama 960 mahakama 803 ndizo zinazofanya kazi na mahakama 157 ni chakavu. Pia mahakama 487 tu ndio zenye mahakimu wa kudumu (wakazi wa eneo la mahakama) na mahakama 316 zina mahakimu wanaotembelea na mahakimu mara moja au mbili kwa wiki. Ili kulinda na kutoa haki ipo haja ya Serikali kuimarisha mifumo ya utoaji haki na utawala wa Sheria kama haki ya Kikatiba chini ya Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977.
Taarifa hii pia imeonyesha changamoto mbalimbali za haki za binadamu ikiwa ni pamoja na hali ya rushwa, elimu, na haki ya kupata maji safi na salama; Hivyo basi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Kinapendekeza yafuatayo
  1. Elimu ya Haki za Binadamu inapaswa kujumuishwa kwenye mfumo wa elimu rasmi wa nchi ili kuweza kukuza uelewa wa haki za binadamu
  2. Serikali inatakiwa kutekeleza mpango wa kitaifa wa haki za binadamu ikishirikiana na wadau wengine kama asasi zisizo za kiserikali na vyombo vya habari
  3. Tunaitaka Serikali kutunga Sheria inayolinda haki za mtoa taarifa ili kuweza kupata ushirikiano wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa
  4. Tunaitaka serikali kutoa kipaumbele katika kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii kama vile maji, umeme, elimu, na afya.
  5. Kuboresha mifumo ya utoaji haki kwa maana mahakama na mabaraza mbali mbali ya utatuzi wa migogoro ili kukuza dhana ya utawala wa sheria
  6. Haki ya kuishi imeonekana ni moja ya haki zinazokiukwa kwa kiwango kikubwa hivyo basi ipo haja ya wadau mbali mbali ikiwa ni pamoja na viongozi wa dini kuiasa jamii kuheshimu haki ya kuishi
  7. Haki za watoto na wanawake ipo haja kwa jamii yetu kulinda na kuheshimu haki hizi za makundi haya muhimu katika jamii ili tuweze kukuza ustawi na maendeleo ya taifa.
Mwisho ninawatakia kila la heri katika harakati na kazi za kueneza na kukuza uelewa wa haki za binadamu na utawala bora ili tuweze kufikia jamii tunayotaamali ya haki na usawa.

Nawashuruku sana kwa kunisikiliza na ushirikiano

Dr. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji - LHRC

No comments:

Post a Comment